Raila aitisha maandamano siku ya uchaguzi

KIONGOZI wa muungano wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga (pichani) ameitisha maandamano ya nchi nzima Oktoba 26, siku ambayo uchaguzi mpya wa urais umepangwa kufanyika.

Raila Odinga ambaye alijitoa katika uchaguzi huo amesisitiza kuwa uchaguzi hauwezi kufanyika bila mabadiliko ndani ya Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo (IEBC) Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati tayari alisema ana mashaka kama uchaguzi huo utakuwa huru na haki iwapo viongozi wa kisiasa nchini humo hawatazungumza na kutatua mzozo wa kisiasa unaoendelea.

Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa nchi itafanya maombi mwisho wa wiki hii kabla ya marudio ya uchaguzi mkuu wiki ijayo. Taarifa ya Rais Kenyatta ilikuja siku moja baada ya mmoja wa makamishna wa juu wa IEBC, Roselyne Akombe, kujiuzulu nafasi yake na kukimbilia Marekani kwa kile alichosema amekuwa akipata vitisho vya kuhatarisha maisha yake.

Rais Kenyatta alisema kuwa Wakenya watatumia mapumziko ya mwisho wa juma hili kwa kufanya maombi na maridhiano kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais ambao umepangwa kufanyika Oktoba 26, mwaka huu.