Wananchi wasifia makubaliano serikali, Barrick

WANANCHI wamesema makubaliano yaliyofi kiwa kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick Gold ni hatua muhimu kwa taifa kuanza kunufaika na rasilimali hiyo.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini aliliambia gazeti hili jana kuwa Rais John Magufuli amethubutu kufanya jambo kubwa, ambalo lilikuwa likiogopwa kwa muda mrefu la kuzungumzia umuhimu wa rasilimali kuwanufaisha wazawa. Alisema hatimaye taifa limethubutu kusema hapana na kuwataka wawekezaji hao kuingia kwenye mazungumzo kuhusu madini hayo.

Alisema makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Barrick ni hatua kubwa ya kusonga mbele katika kusimamia rasilimali za nchi. “Kwa mara ya kwanza tumefanikiwa kukutana na kuzungumza na watu ambao zamani tulikuwa tukiwaogopa. Baadhi ya watu walimbeza Rais Magufuli kuwa eti tutashitakiwa, tutafilisiwa lakini hatimaye leo muafaka umepatikana,” alisema Askofu Kilaini.

Kuhusu kamati hiyo ya majadiliano iliyoongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Askofu Kilaini alisema inapaswa kupongezwa kwa kazi nzuri na uzalendo walioonesha katika kuhakikisha kuwa mazungumzo hayo yanazaa matunda. Kwa upande wake, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika mazungumzo hayo, Taifa linapaswa kuendelea kutafakari zaidi kuhusu hali yake ya kiuchumi.

Dk Bashiru alisema kuwa ni jambo jema kuwa na sheria ya madini inayoipa nguvu Serikali, Bunge na wananchi katika kusimamia rasilimali ya madini, lakini ili taifa liondokane na udumavu wa kimaendeleo linapaswa kuwekeza zaidi kwenye mambo yanayowezekana kwa urahisi kama vile kilimo, ufugaji na viwanda. “Uwezo wetu wa kuwekeza kwenye sekta ya madini ni mdogo.

Kwenye madini kunahitajika teknolojia na mtaji mambo ambayo kwa kiasi kikubwa hatuna uwezo nayo. Vita ya uchumi bado mbichi, hatua ya Rais ya kushughulikia matatizo hayo itupe funzo katika kutoka hapo na tujikite zaidi kwenye kujitegemea kwa kuzalisha vitu ambavyo tuna uwezo navyo kama vile sukari, nguo na vyakula,” alieleza Dk Bashiru.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mabenki nchini (TIOB), Patrick Mususa alisema kuwa makubaliano hayo yanatia moyo kwa kuwa nchi ilikuwa imeibiwa na kuonewa. Alisema hayo ni matumaini mapya kwa kuwa nchi iliumia kutokana na kuwa na misingi mibovu, mipango mibovu na sheria kandamizi za madini dhidi ya wananchi ambazo ziliwabeba zaidi wawekezaji.

“Barrick imekubali kulipa zaidi Sh bilioni 700, itaisaidia Serikali katika kutoa huduma za jamii kama ujenzi wa miundombinu, elimu na afya. Lakini pia gawio la 50 kwa 50 ya faida itakayotokana na madini hayo pia litainufaisha sana taifa ikilinganishwa na ilivyokuwa awali,”alisema Mususa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano hayo kati ya Serikali na Barrick, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alitaja malengo ya Serikali katika majadiliano hayo na baadhi yake ni kuainisha fidia kutokana na makosa mbalimbali yaliyofanywa na makampuni tanzu ya Barrick nchini, kujadili na kuweka mfumo mpya wa uendeshaji wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ili kuleta mgao sawa wa mapato kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick.

Malengo mengine ni kujadili na kukubaliana muundo na mfumo wa uendeshajii utakaoiwezesha Tanzania kupata manufaa zaidi kutokana na uwekezaji unaofanywa na migodi, kubadilisha mikataba ya uendeshaji migodi ili iendane na marekebisho ya sheria ya madini. Ikumbukwe kwamba Rais Magufuli aliunda Tume mbili za kuchunguza biashara ya madini.

Tume ya kwanza iliongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma iliyoanza kazi Machi 29 hadi Mei 24 mwaka huu. Tume ya pili iliongozwa na Profesa Nehemiah Osoro iliyoanza kazi Aprili 11 hadi Juni 12 mwaka huu na kisha akaunda Kamati ya Majadiliano iliyoongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof Palagamba Kabudi ambayo iliwasilisha taarifa yake kwa Rais jana.