Rais China aahidi ushirikiano zaidi

RAIS wa China, Xi Jinping amefungua Mkutano Mkuu wa 19 wa Chama tawala cha Kikomunisti (CPC) na kuahidi nchi hiyo haitafunga milango ya ushirikiano na nchi nyingine duniani bali kuuendeleza zaidi.

Mkutano huo unaofanyika wakati Rais huyo akimaliza awamu ya kwanza ya kipindi cha utawala cha miaka mitano. Alitumia saa tatu na nusu kuelezea mafanikio aliyopata ikiwemo kuongeza pato la Taifa. Rais JinPing alisema wakati akiingia madarakani mwaka 2012, alikuta Pato la Taifa la China likiwa ni fedha za nchi hiyoYuan trilioni 54 kwa mwaka na sasa pato hilo ni karibu Yuan trilioni 80.

Inaelezwa kuwa kuongezeka kwa pato hilo la taifa kunaashiria nchi hiyo kufikia lengo lake la kuwa taifa lenye uchumi mkubwa duniani. Mbali na kuongeza Pato la Taifa, pia amejivunia kuwaondoa wananchi wa nchi hiyo ya pili kwa uchumi mkubwa duniani zaidi ya milioni 60 katika hali ya umaskini kwa kipindi hicho cha miaka mitano.

Mkutano huo wa siku nne unatarajiwa kutoa mrithi wa nafasi ya urais kama katiba ya chama hicho inavyosema kuwa baada ya miaka mitano, rais aliyepo madarakani anapaswa kumtangaza mrithi wake pamoja na kuchagua viongozi wengine wa ngazi mbalimbali wa chama hicho watakaoongoza nchi hiyo. Katika mkutano huo unaofuatiliwa na watu mbalimbali duniani, mageuzi ya Katiba ya chama hicho yanayolenga kukabiliana na mabadiliko ya mazingira na hali ilivyo kwa sasa yaliwasilishwa rasmi.

“Uzoefu unaonesha kufanya marekebisho ya katiba ya chama kwa maendeleo endelevu na majukumu yaliyopo itasaidia kila mwanachama kuelewa, kutumia na kutekeleza katiba ya chama,” alisema Rais Xi. Katika suala la ushirikiano na nchi mbalimbali duniani, Rais Xi alisema wataendelea kuheshimu uhuru wa mataifa rafiki na kudumisha uadilifu wa mipaka wa mataifa huku wakiandaa mipango ya ushirikiano na kuendeleza miradi ya ushirikiano kwa kutumia majadiliano.

“China itafungua milango ya bidhaa kutoka mataifa rafiki na kulinda haki za kimsingi za wawekezaji wa nje,” alisema. Alisema uchumi wa nchi hiyo umekuwa ukibadilika kutoka kukua kwa kasi hadi kiwango cha ubora wa hali ya juu kimaendeleo kwa kuendeleza uchumi wa kisasa hivyo lazima wazingatia hali halisi ya uchumi wa ndani.

Alisema Serikali yake itawezesha mtaji wa taifa kuwa thabiti, imara na kukua zaidi na kuwezesha kampuni za uwekezaji kutoka China kufikia viwango vya kimataifa na ushindani mkubwa ulimwenguni. “China itazingatia jukumu lake la kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini humo na kuboresha mfumo wa usimamizi inayounganishwa na sera ya fedha,”alisema. Katika kukiimarisha chama, alisema kitaendelea kuimarisha vita dhidi ya vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanapata ushindi katika vita hivyo.

Alisema katika mfumo wa utawala wa ujamaa, wanazingatia itikadi za Kichina pamoja na kuwa na taifa linalotekeleza mfumo wa kikomunisti. Mkutano huo ulioanza jana, unajumuisha wajumbe zaidi ya 2,307 wanaotoka katika ngazi mbalimbali za kijamii kutoka taaluma na nyanja mbalimbali wakiwemo wachumi, sayansi na teknolojia, ulinzi na usalama, mahakama, elimu, utamaduni, michezo, wakulima na viongozi mbalimbali katika jamii. Pia watachagua viongozi katika kamati mbalimbali za maamuzi za CPC yenye wanachama wanaokadiriwa kuwa milioni 89.44 kwa mujibu wa takwimu zao za mwaka jana.