UVCCM wafurahia utendaji kazi wa JPM

KASI ya utendaji wa Rais John Magufuli (pichani) imelikuna Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ambao wamempongeza na kumtaka aendelee na utendaji huo bora.

Akizungumza na wandishi wa habari, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera, Yahaya Kateme alisema Baraza la Vijana limefurahishwa na utendaji wa Rais, hasa katika kuondoa kero za wananchi na hivyo kupunguza maswali.

“Rais amefanya mabadiliko mbalimbali yakiwemo ya kudhibiti utendaji wa watumishi wa umma ofisini, kutoa elimu bure, kutoa mikopo kwa wanafunzi, ukusanyaji kodi, utoaji huduma na kufufua mashirika mbalimbali pamoja na kuanzisha viwanda,” alisema.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana (UVCCM), Sylevester Yaredi alimpongeza Rais Magufuli pia kwa kuwaamini vijana na kuwapa nafasi nyingi za uongozi nchini, akaomba vijana nao wafanye kazi vizuri ili kuonesha shukrani kwa kiongozi huyo aliyewateua.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya na Songwe, Amani Kajuna alisema bado kuna kero chache zikiwemo za maji na umeme vijijini, hivyo wanamwomba Rais ahakikishe wahusika wa wizara sekta hizo wanaondoa kero hizo.