Mawaziri kueleza mafanikio ya wizara zao TBC I

KUANZIA leo hadi Desemba 28, mwaka huu, mawaziri watazungumzia utekelezaji wa sera,miradi na mafanikio ya wizara zao kupitia kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na kituo cha runinga,TBC1.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas ilisema kipindi hicho ni cha mkakati wa kuimarisha mawasiliano ya Serikali kwa umma.

Dk Abbasi alisema kwa mwaka wa fedha 2017/18, kipindi hicho kitawahusisha mawaziri wa wizara mbalimbali na kwa kipindi cha leo kinachorushwa kuanzia saa tatu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo atazungumzia wizara yake.

“Wananchi mnaombwa kufuatilia kipindi hicho na vipindi vingine vya Tunatekeleza ambavyo hurushwa Jumatatu na Alhamisi ili mfahamu mipango ya serikali na nama inavyosimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema Dk Abbasi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari nchini.

Dk Abbas alisema awali kipindi kilihusisha makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa taasisi na idara zinazojitegemea za Serikali na walieleza wanavyotekeleza miradi ya maendeleo sasa zamu ya mawaziri.