Zabuni Stiegler’s Gorge kufunguliwa Novemba 6

SERIKALI imesema zabuni za kampuni zinazoomba kujenga mradi wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge Mto Rufi ji mkoani Pwani, zitafunguliwa rasmi Novemba 6, mwaka huu.

Mradi huo unaotarajia kuzalisha megawati 2,100, utaanza baada ya kumpata mkandarasi baada ya kazi ya zabuni kukamilika. Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliliambia gazeti hili jana kuwa mchakato wa kupokea zabuni kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo wa umeme wa Stiegler’s Gorge, bado unaendelea na waombaji wote watajulikana mwezi ujao wakati zabuni hizo zikifunguliwa.

Kwa mujibu wa Mgalu, mpaka Oktoba 11, mwaka huu, kampuni zilizoomba zabuni hiyo zilikuwa 79 na bado nyingine zinaendelea kuomba. Alisema kati ya kampuni hizo 79, kampuni moja inatoka nchini Misri. “Tutazifungua zabuni tarehe sita mwezi ujao na baada ya hapo tuzifanyia tathimini ili kumpata mkandarasi aliyekidhi vigezo. Tukishampata tutaingia naye mkataba na kumkabidhi mradi ili aanze kazi,” alieleza Mgalu.

Alisema uwezo wa kuzalisha umeme kwa sasa kutoka katika vyanzo vilivyopo ni megawati 1,450. Naibu Waziri aliongeza kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuzalisha megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020.

Alisema megawati hizo zitatokana na vyanzo vilivyopo, kama vile maji, mafuta na gesi asilia. “Kidatu inazalisha megawati 204, Kinyerezi I inazalisha megawati 150, lakini ‘extension’ ya Kinyerezi I itakapokamilika mwaka 2019, itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 185, kwa hiyo Kinyerezi I yote itakuwa ikizalisha jumla ya megawati 335,” alisema Mgalu. Mgalu aliongeza kuwa Kinyerezi II inatarajiwa kukamilika mwakani na itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 240.

Alisema lengo la serikali ni kuzalisha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025. Katika hotuba zake, Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa serikali yake lazima itajenga mradi huo wa Stiegler’s Gorge kwa kuwa ndiyo ilikuwa ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Rais Magufuli amekuwa akisema kuwa serikali yake imejikita kwenye uchumi wa viwanda ambavyo vinahitaji umeme wa kutosha na wa uhakika. Ili kufikia azma ya kuwa na viwanda vingi na vya aina mbalimbali na kulifanya taifa kufikia uchumi wa kati, Rais amekuwa akisema kuwa serikali lazima ijenge mradi huo wa Stiegler’s Gorge.