Bil. 400/- zatolewa mikopo vyuo vikuu

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa mikopo kwa wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/18 katika awamu ya kwanza.

Kwa mujibu wa tarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, jumla ya Sh bilioni 34.6 zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao 10,196. Badru alisema kwa ujumla ya Sh bilioni 108.8 zitatolewa kwa wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/2018.

“Orodha hiyo ya kwanzainapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo (www. heslb.go.tz) na itatumwa kwa vyuo husika. Orodha nyingine (batches) zitafuata kadri taratibu za udahili na uchambuzi zinavyokamilika,” alisema Badru. Alisema lengo la bodi hiyo ni kutoa majina ya wote waliofanikiwa kupata mkopo kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu.

Vyuo zinafunguliwa Oktoba 30. Alieleza kuwa orodha hiyo ya wanafunzi 10,196 imepatikana baada ya kupokea na kuchambua awamu ya kwanza ya majina ya wanafunzi 32,495 waliopata udahili katika chuo kimoja.

“Itakumbukwa kuwa moja ya sifa kuu za kupata mkopo ni mwombaji kupata udahili katika taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na serikali. Wanafunzi waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja na ambao wana sifa za kupata mikopo, watapangiwa mikopo baada ya kuchagua na kuthibitisha chuo watakachojiunga kwa ajili ya masomo,” alisisitiza mtendaji huyo wa HESLB.

Pamoja na hayo, alibainisha kuwa katika mwaka huo wa masomo wa 2017/18, bodi pia imetenga kiasi cha Sh bilioni 318.6 kwa ajili ya wanafunzi wanaoendelea na masomo. Alisema fedha hizo za mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo, zimeanza kuanza kutumwa kwa wanafunzi kuanzia jana. Alisema jumla ya wanafunzi wanaoendelea na masomo yao, 93,295 ndio wanaotarajiwa kutumiwa fedha hizo za mikopo Sh bilioni 318.6.

“Tayari serikali imeshatoa fedha hizo na lengo la bodi ni kuhakikisha fedha zinafika vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ili kuwaondoloea wanafunzi usumbufu,” alifafanua. Alisema Bodi ya Mikopo inawasihi waombaji wa mikopo kuwa na subira wakati ikiendelea kukamilisha maandalizi ya orodha zinazofuata za wanafunzi waliopata mikopo.

Kwa mwaka wa masomo 2016/17, jumla ya wanafunzi waliopatiwa mikopo baada ya uchambuzi wa maombi kukamilika ni 20,183 wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 93,295 ambao wana sifa mbalimbali. Aidha, kiasi cha fedha zilizotolewa kwa mwaka 2015/2016 kwa ajili ya mikopo hiyo ni Sh bilioni 459 na kimetolewa kwa wanafunzi 122,486.

Takwimu za mwaka 2014/2015 zinaonesha mwaka huo, ndiyo ulikuwa ukiongoza kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha, ambapo walitoa kiasi cha Sh bilioni 341 kwa wanafunzi 99,069 na mara ya kwanza bodi hiyo kutoa mikopo ilikuwa ni mwaka 2005/2006 ambao walitoa kiasi cha Sh milioni 56.1 kwa wanafunzi 42,729. Pamoja na utolewaji wa mikopo hiyo, mpaka sasa serikali imetoa Sh trilioni 3.1 tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo, lakini ni Sh milioni 217 pekee zilizorejeshwa huku Sh bilioni 588 zikiwa zimefikia muda wake zikitakiwa kulipwa.