Mbaroni kwa tuhuma za kumchinja mumewe

MKAZI wa Kata ya Tinde katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Zena Mohamedi (28) anashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumuua mumewe, Bakari Salehe (35) kwa kumchinja shingo kwa madai ya wivu wa kimapenzi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Simon Haule alisema tukio hilo limetokea juzi saa 2.30 usiku wakati mwanamke huyo akiwa na mume wake nyumbani kwao, simu ya mwanamume iliita ndipo akaichukua mkewe huyo na alipoipokea akasikia sauti ya mwanamke, na ndipo ugomvi na majibizano yalipoanzia.

Kamanda Haule alisema baada ya ugomvi huo kuzuka, ndipo mwanamke alipochukua kitu chenye ncha kali na kumchinja shingo mume wake na kusababisha kupoteza maisha, na mwili wake tayari umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

“Chanzo cha tukio hili ni wivu wa kimapenzi ambapo mwanamke mara baada ya kuita simu ya mumewe aliikimbilia kuipokea, na aliposikia sauti ya mwanamke mwingine kwa hisia zake akaona tayari ni hawara wa mume wake, ndipo wakaanza kupigana hadi kusababisha kifo,” alisema Haule.

Hata hivyo, Kamanda Haule alisema jeshi hilo linamshikilia mwanamke huyo kwa mahojiano zaidi na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu shitaka la mauaji lililotokea na kutumia kitu chenye ncha kali. Aidha, kamanda alitoa mwito kwa wananchi kuacha tabia za ugomvi wakutumia vitu vyenye ncha kali.